NENO LA SIKU.
Na, Mama Eliakunda Mwingira - Kanisa La Efatha
TAREHE: 19/11/2024
SOMO: NAMNA YA KUFIKIA BARAKA ZETU KATIKA KUTII MAAGIZO
Isaya 1:19 “Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;”
Utii maana yake ni nini? Ni kufanya sawa bila maswali, utii ni amri haibadiliki, utii ni sheria, kutii ni lazima hakuna mjadala; kama hauwezi kumtii Mungu na kuzitii sheria zake basi hautaweza kutiisha chochote kikakutii hapa chini ya jua.
Kukosa utii ni sawa na kuwa na shoka ambalo halina mpini.
Yakobo 4:7 “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.” Usipomtii Mungu kamwe hautaweza kumkimbiza ibilisi na yeye akakimbia, bali atakaa nyumbani kwako, kazini kwako, kwenye biashara zako na kila mahali katika maisha yako, kwa nini? Kwa sababu wewe sio mtii hivyo hauwezi kumtiisha.
Unakuta vitu haviendi kwa sababu wewe mwenyewe haujakubali kumtii Mungu hivyo ibilisi hawezi kuondoka katika maisha yako.
Mungu ndiye mwenye vyote unavyovihitaji, ana mume/ mke wako, watoto wako kazi au biashara nzuri unayoitaka, sasa kama hauwezi kumtii, je! Utavipataje hivyo?
Utajuaje kuwa hauna utii? Uwepo wa ibilisi utakuwa na wewe, atakusumbua kupitia magonjwa, umasikini, ukata na mateso ya kila aina, utakuwa mtu uliyekwama katika kila unachokifanya hakiendi.
Walokole sisi ni hodari sana kusema shindwa shetani, toka, lakini unapaswa kujua kuwa usipotii hata ukikemea ibilisi anakuangalia tu wala hashituki, neno linasema mtii Mungu halafu ukifika katika kumpinga ibilisi wala hautumii nguvu.