SOMO: UKOMBOZI KAMILI KUPITIA NENO.
Ukombozi maana yake ni kutoka katika maumivu, mateso na makandamizo. Ukombozi unahusisha mwili, roho na nafsi. Lengo la kukombolewa ni kurejeshwa katika furaha ya uumbaji maana hatukuumbwa ili tuteseke.
Maumivu au mateso unayopitia ni matokeo ya makosa au dhambi yako mwenyewe au wazazi wako. Maombolezo 5:7, "Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao."
Furaha ya kwanza ya uumbaji inaanzia pale mtu anapoelewa sheria ya MUNGU. Ukombozi ni urejesho wa mtu kwenye nafasi yake ya kufurahia wokovu na maisha.
Isaya 35:10, "Na hao waliokombolewa na BWANA watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia."
Dalili ya kwamba umepokea ukombozi ni pale unapotamani na kuwa na shauku ya kufanya ibada kila wakati. Kiu ya ibada inakupa kuondoka kwenye maumivu ya uovu na dhambi. Furaha ya milele itakuandama wewe na uzao wako, kazi zako, utumishi wako, afya yako na baraka zako zote.
Kuna njia nyingi za kupokea ukombozi, mojawapo ya njia hizo ni kupitia neno. Kwanini neno linaleta ukombozi? Neno linaleta ukombozi kwa sababu;
1. Neno linabeba utakaso wa kila unajisi ambao unaweza kukupata kupitia kuzaliwa au kwa maneno ya kunuiza na laana. Unapopokea neno, umepokea utakaso wako. Yohana 17:17, "Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli."
2. Neno linaweza kuumba chochote. Ukijua kutumia neno utaumba uzao wako na chochote unachohitaji.
Zaburi 33:6, "Kwa neno la BWANA mbingu zilifanyika, Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake."
3. Ni ushuhuda na ushindi dhidi ya washitaki wako wote. Mtu yeyote mwenye neno, anatangaza ushindi katikati ya changamoto na mitego ya adui.
Ufunuo wa Yohana 12:10-11, "Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.
Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa."
:-MCHUNGAJI JAMES JOSEPHAT NYANSIKA- KANISA LA EFATHA MWANZA.
... See MoreSee Less